UNA Tanzania kuongoza zoezi la utengenezaji wa Mwongozo wa Utoaji na Urejeshwaji wa Mikopo ya Asilimia 10% Tanzania

Katika kufikia maendeleo ya pamoja haswa katika kuhakikisha makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu yana nufaika na mikopo ya asilimia 10% isiyo na riba UNA Tanzania kuongoza zoezi la uandaaji wa Muongozo wa utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10%. Kazi hii ni muendelezo wa kazi za UNA Tanzania katika kuhakikisha kua fedha za mikopo isiyo na riba zinanufaisha makundi ya Wanawake, Vijana na Walemavu. katika kuanzisha shughuli za kimaendeleo na kuiingizia kipato kama vile biashara,ufugaji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Hatua hii ni muendelezo wa kufanikisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa iliyo fanyiwa marekebisho katika ya mwaka 2018 (Cap 290, Section 37A). Marekebisho haya yanazitaka halmashauri zote nchini kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao ya ndani kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Marekebisho hayo ya sheria yalifuatiwa na utungaji wa kanuni zinazoainisha masharti, vigezo vya utoaji na usimamizi wa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi hivyo.

Mnamo tarehe 13/10/2020 UNA Tanzania pamoja na Policy Forum walishiriki kikao cha kimkakati kilichofanyika na Uongozi wa Idara ya Serikali za Mitaa (Tamisemi). Katika kikao hiki ilibainishwa kwamba ijapokua kuna sheria na kanuni zinazo simamia uratibu wa mikopo hii katika ngazi za halmashauri, bado kuna changamoto nyingi zinazokabili mfumo na utaratibu wa utoaji na usimamiaji wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini. Akielezea kuhusu changamoto hizo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa, Bi Angelista Kihaga, alieleza kuwa licha ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 91 kutolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, bado kuna  tatizo la usimamizi na uwepo wa vikundi hewa. Alieleza kuwa wasimamizi wengi hawana ujuzi wa kutosha wa kusimamia vikundi ili viweze kutekeleza shughuli zake za maendeleo ziwe endelevu na pia ziweze kuzalisha fedha ambazo zitarejeshwa katika Halmashauri husika. Alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwajengea uwezo wasimamizi hao ili kuleta tija za mikopo wanayopatiwa wanavikundi.

Changamoto kama, ukosefu wa fedha na ujuzi wa kufanya ufuatiliaji kwa vikundi vilivyopata mikopo ilielezwa kama moja ya changamoto zinazokabili Halmashauri nchini. Changamoto hii inaenda sambamba na ukosefu wa vitendea kazi vya kitaalamu hasa ngamizi (computer) kwa ajili ya utunzaji wa kumbumbuku ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa. Bi Kiaga alitanabaisha kuwa pia, kunahitajika kuendelea kutolewa kwa mafunzo kwa vikundi jinsi ya kufanya shughuli za kijasiriamali ili vikundi hivyo viwe na mafanikio katika miradi yao na iwe endelevu ambayo itasaidia kukuza kipato cha wana kikundi na kuwezesha urejeshwaji mikopo hiyo kwa wakati na kwa ufanisi.

Akizungumzia kuhusu namna ya kutatua changamoto zilizopo katika kusimamia shughuli na mfumo wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo, Afisa wa UNA Tanzania ambao wataongoza zoezi la uuandaaji wa muongozo, bwana Lucas alieleza kua kutokuwepo kwa muongozo ambao utaleta utekelezaji makini wa kanuni na sheria ni sehemu ya changamoto za uendeshaji wa Mikopo hii. Akisisitiza katika hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa Dk. Charles Mhina alisema kuwa kuwepo kwa kanuni na sheria zinazosimamia mikopo hii ya 10% hata hivyo kuna uhitaji wa kua na muongozo ambao utaonyesha namna bora zaidi na kusaidia kutoa tafsiri ya ndani zaidi na kutoa maelekezo rafiki katika itekelezaji wa kanuni hizo. Alitolea mfano kuhusu muundo wa vikundi amabao nao unatakiwa kuangaliwa ili kuhakikisha vikundi hivi vinafanya kazi kama zilivyo ainishwa kwenye uchanganuzi wa wazo la biashara. Pia alisisitiza kuwa ni muhimu kundaa mwongozo bora ambao utawezesha  zoezi la utoaji na urudishaji wa mikopo kuwa rahisi na lenye tija kwa vikundi vinavyo nufaika  na kusaidia uelewa wa urejeshwaji wa fedha hizo ambo umekua ni changamoto kubwa.

Akizunguza katika kujibu hoja moja wapo iliyo tolewa na Mratibu kuhusu UNA Tanzania, ambae aligusia kuhusu mabadiliko katika kanuni, Dk Mhina alieleza kwa ufasaha kuwa Serikali imesha andaa rasimu ya kurekebisha kanuni zilizopo zinazoratibu utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Mabadiliko haya ya kanuni ni sehemu yanabeba maono ya muda mrefu ya UNA Tanzania ambayo yaliwasilishwa TAMISEMI katika vipindi kadha wa kadha. Alibainisha kua mabadiliko haya ni katika kuhakikisha kanuni zinakua rafiki na zenye kuleta tija katika utoaji wa mikopo hii isiyo na Riba. Hata hivyo alidokeza kuwa ni muhimu kuwa “ili tuweze kuwa na mwongozo bora lazima tuwe na kanuni ambazo zipo imara”. 

Katika kufunga kikao hicho maazimio yaliwekwa ikiwemo kuundwa kwa kikosi kazi cha uandaaji wa muongozo ambacho kitaongozwa na UNA Tanzania alie kabidhiwa jukumu la kusimamia na kuhakikisha mchakato unakamilika kwa wakati. Kikundi kazi kitajumuisha wadau kutoka Tamisemi na Policy Forum pamoja na wadau wengine ambao watakaa pamoja ndani ya siku thelathini (30) na kuandaa mwongozo ambao utajumuisha mawazo ya wadau wengine. Mwongozo huo utakapokamilika, utasambazwa katika ngazi husika ili kurahisisha na kuweka ufanisi zaidi katika mfumo wa utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini.